UWSA SACCOS LTD ilisajiliwa tarehe 03 Machi 2014 ikiwa na Wanachama 140 na hisa zenye thamani ya Shilingi 6,240,000/=. Thamani ya Hisa imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka ambapo kufikia 2020 chama kimekuwa na na hisa zenye thamani ya Shilingi 62,315,000/=.
Ongezeko la thamani za Hisa limechangiwa na kuongezeka kwa Wanachama wa SACCOS kufikia 148. Hata hivyo, ongezeko la Wanachama limesababisha kuwepo kwa changamoto ya utoaji huduma iliyo bora na hivyo chama kulazimika kuwa na Sera na Miongozo mbalimbali itakayosaidia utoaji wa huduma bora kwa manufaa ya chama na Wanachama wenyewe.
UWSA SACCOS LTD ni Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo kilichosajiliwa kwa namba 914MBR. Chama hiki kilianzishwa mahususi ili kusaidia watumishi waajiriwa wa Mamlaka ya Majisafi na usafi wa Mazingira Mbeya.
Chama hiki kina jumla ya Wanachama 148 ikiwa wanaume ni 88 na wanawake ni 60 wenye jumla ya Hisa zenye thamani ya Shilingi 62,315,000/=.
UWSA SACCOS LTD, inatoa huduma mbalimbali kwa wanachama wake. Miongoni mwa huduma hizo ni utoaji wa mikopo kwa Wanachama (Mikopo ya maendeleo, Mikopo ya Elimu na Mikopo ya Dharura). Aidha, wanachama wananufaika na chama kupitia huduma nyingine za kijamii ambazo ni utoaji wa Mkono wa Kwaheri ama rambirambi kwa mfiwa na fao la Kustaafu.
Hadi kufikia mwaka 2022, Chama kimekuza mtaji wake hadi kufikia Shilingi Milioni 350 ikiwa ni mjumuisho wa Hisa na Akiba za Wanachama.
Chama kina vyanzo mbalimbali vya mapato. Vyanzo vya mapato vya Chama ni pamoja na uuzaji wa fomu za mikopo kwa wanachama, riba itokanayo na mikopo na adhabu mbalimbali wanazotozwa wanachama.
UWSA SACCOS LTD inatoa huduma zake kwa usawa, haki, kwa mujibu wa sheria za ushirika, kanuni za huduma ndogo za fedha na kwa kuzingatia miongozo mbalimbali ya vyama vya Ushirika. Aidha, Chama kinaongozwa na Bodi ya Chama ikiongozwa na Mwenyekiti, Katibu na Mtunza Hazina kwa Mujibu wa Sheria, Taratibu na Kanuni (STK) kwa kuzingatia Masharti ya Chama na utawala bora. Hata hivyo, ili kutekeleza mipango yake Chama kinafanya shughuli zake chini ya Kamati mbili ambazo ni Kamati ya Usimamizi na Mikopo.
Dira ya Chama ni; Kuwa Chama bora cha akiba na mikopo chenye kutoa huduma bora na riba nafuu kwa Wanachama wake nchini Tanzania.
Dhima ya Chama ni; Kutoa huduma bora ya utunzaji wa akiba za Wanachama, kutoa mikopo kwa Wanachama na kutoa elimu dhidi ya matumizi ya fedha kwa wakati kwa nia ya kuwajengea wanachama uchumi bora.
Ushirikiano/Mshikamano(Solidarity) Viongozi wa Chama, Wanachama na Watendaji wanapaswa kuwajibika kwa masilahi mapana ya Chama.
Uwajibikaji (self responsibility) Mafanikio ya Chama yatafikiwa endapo kutakuwepo na ushirikiano na mshikamano wa karibu kati ya Wanachama, Bodi ya watendaji na wadau wengine. Ni wajibu wa kila mdau kutoa Ushirikiano pale inapohitajika kufanya hivyo.
Kujali Wanachama Mara zote Viongozi wa Chama pamoja na Watendaji watapaswa kutoa huduma iliyo bora kwa Wanachama wake.
Uwazi Shughuli za Chama zitaendeshwa katika hali ya uwazi kwa kuzingatia misingi ya kumlinda Mwanachama (consumer protection) pamoja na kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya chama.
Ustadi Bodi pamoja na watendaji watapaswa kuzingatia na kufuata viwango vya kitaalamu walivyonavyo wakati wa kuendesha shughuli za Chama.
Uaminifu (Honesty) Viongozi wa chama pamoja na watendaji wanapaswa kuwa waaminifu wakati wa kuendesha shughuli za Chama.
Kujitolea na kujitegemea(self help) Viongozi wa chama na watendaji wanahamasishwa kuwa na moyo wa kujitolea na kujitegemea wakati wote kwa manufaa ya Chama na Wanachama wake.
Usawa Viongozi wa Chama pamoja na Watendaji wanapaswa kuwa waadilifu wakati wa kuendesha shughuli za Chama.
Uadilifu Viongozi wa Chama pamoja na Watendaji wanapaswa kutoa huduma kwa Wanachama Wote pasipo upendeleo wowote, kwa Mujibu wa Sera, Taratibu na Kanuni za Chama.